Ujapo kwasika, mtulivu uwe
Alipenda Rabuka, nilivyo niwe
Ikujiapo fanaka, adilika wewe
Alinipa kumbi, alekupa Kiti
Kazi niitendayo, yanikimu daima
Naipenda hiyo, iwapo ni rukwama
Yangu kazi hiyo, wewe ipe heshima
Alinipa kumbi, alekupa Kiti
Manani kanipa, hii yangu sura
We heshima nipa, niwapo chotara
Kama baya kanipa, nawe nzuri sura
Alinipa kumbi, alekupa Kiti
Nikaapo pale, paheshimu wewe
Kibadangu kile, chakuhusu ni we?
Shukuru Molale, kwa ulipo wewe
Alinipa kumbi, alekupa Kiti
Hata kama mie, sikupata elimu
Si penzi langu wee, kut’ona mwalimu
Tulivyo tukae, sote binadamu
Alinipa kumbi, alekupa kiti
Kafanya duniani, tufautiane
Lengole Manani, zoteni Karne
Sote duniani, tushirikiane
Alinipa kumbi, alekupa Kiti.
No comments:
Post a Comment